DC Mgandilwa asema ufaulu lazima uongezeke....
Wazazi wasio wafatilia maendeleo ya watoto wao shule na kuwaozesha kuishia jela...
Tarehe 17/9/2016 Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Mh. Hashim Mgandilwa alikutana na wadau wa Elimu Kigamboni kujadili changamoto za elimu na kupendekeza namna ya kuzitatua.
Waliohudhuria ni pamoja na wadau wa elimu Kigamboni, wanafunzi wa vyuo, Wahitimu wa Vyuo, na wadau wa maendeleo waliopo ndani na nje ya wilaya ya Kigamboni.
Baada ya Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Mh. Mgandilwa kutoa hali halisi ya hali ya elimu wilayani humo, kabla ya kuwakaribisha wadau kwa michango na maoni yao alikemea baadhi ya mambo ambayo yanafanywa na wazazi yanayorudisha nyuma maendeleo ya kitaaluma kwa watoto wao.
"......kuanzia sasa mzazi atakayeshiriki kumuachisha shule na kumuozesha mtoto wake atachukuliwa hatua kali za kisheria....., watoto wote lazima tuhakikishe wanasoma na kumaliza..... " Alisema DC Mgandilwa.
Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Mh. Hashim Mgandilwa akizungumza na wadau wa Elimu, Kulia ni Mama Mpangala Kaimu Afisa Elimu ya Sekondari Wilayani humo
Pia aliongeza kuwa manispaa ya Kigamboni iko mbioni kutengeneza Sheria ndogondogo zitakazowabana wazazi kufatilia mienendo na maendeleo ya watoto wao mashuleni.
".....haiwezekani serikali inachukua hatua za makusudi za kuwapa elimu bure, kuwapa madawati ya kutosha, kujenga vyumba vya madarasa na mahabara alafu wewe mzazi ushindwe kufatilia mtoto wako kama anafika shule au unaishia beach na kwenye makundi ya kihuni akifeli unaanza kulaumu serikali...." alionya DC Mgandilwa.
Baadae Mkuu wa wilaya alitoa nafasi kwa wadau waliohudhuria kuchangia kwa Uhuru na kupendekeza namna gani ya kuboresha elimu Kigamboni. DC Mgandilwa alisema Ofisi yake ingeweza kufanya maamuzi lakini amewashirikisha wadau ili waone hili ni jambo lao wenyewe, washirikiane katika kuboresha elimu.
Baada ya maoni na michango mbalimbali kikao hicho chini ya Mkuu wa Wilaya kilifikia maazimio. Maazimio ya Muda mfupi ni pamoja na:-
i). Kuanzisha mfuko wa elimu Kigamboni ambao utasaidia kutatua dharula za kielimu kwa wakati pindi zinapotokea kuliko kusubiri na kuomba pesa serikalini.
ii) Kuimarisha idara ya ukaguzi wa shule ili kuwafanya wahusika kuwajibika zaidi na kufanya shule zitekeleze adhima iliyokusudiwa kwa ufanisi.
iii) Kuanzisha mitihani ya ujirani mwema ili kuongeza ushindani miongoni mwa wanafunzi.
iv) Kuanzisha Solving Special Program. Hii italenga kuwafanya wahitimu na wanavyuo kujitolea kufanya solving ya maswali mbalimbali na kuwapa mbinu za kujibu mitihani wanafunzi hasa kwa kuanzia na walio kidato cha nne sasa hivi ili kupunguza Failures.
Hii itajikita zaidi katika masomo ya sayansi na biashara.
Maazimio ya Mipango ya muda mrefu ni:-
i) Kutumia Walimu wa sayansi watakaokuwepo kufundisha shule zaidi ya moja ili kuziba upungufu kwa shule zisizo na Walimu hao kabisa.
ii) Kufanya mitihani ya kila wiki ili kuwajengea wanafunzi tabia za kujisomea kila mara.
iii) DC kukamilisha mpango wake wa kutengeneza forum ya wasomi Kigamboni wenye taaluma mbalimbali watakaosaidia kuboresha sekta ya elimu.
iv) Maandalizi ya kutengeneza Makataba ya Mtandaoni (E-library) itakayosaidia wanafunzi kupata vitabu vyote kwenye mtandao na kujisomea ndani ya maktaba hiyo. Hii itaendana na ukuaji wa sayansi na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA)
v) Ujenzi wa mabweni ya wanafunzi kwenye shule zenye uhitaji huo ili wanafunzi wakae shuleni na kupata muda wa kutosha kujisomea.
Kwa mujibu wa tamko la DC Mgandilwa Maazimio ya Muda mfupi yaliyofikiwa yataanza kutekelezwa mara moja.
Aidha, wadau wa elimu, maendeleo ya Kigamboni na yeyote anayeguswa ambaye hakuweza kufika kikaoni hapo DC Mgandilwa alisema kuwa asisite kufika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Kigamboni kupeleka maoni yake au kupeleka taarifa zake ili ashirikishwe kwenye Forum ya wasomi Kigamboni. Pia anaweza kutuma maoni na taarifa zake kwenda 0719828676 zitapokelewa na kufanyiwa kazi.wa
Katibu tawala wa Wilaya ya Kigamboni Bw. Cosmas Hinju akizungumza na wadau wa Elimu
Wadau wakiwa kikaoni
Wadau wakiwa kikaoni
Wadau wakiwa kikaoni