Tuesday, September 20, 2016

TANESCO KIGAMBONI MALIZA TATIZO LA KUKATIKA UMEME - DC Mgandilwa

Leo tarehe 20/9/2016 Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Mh Hashim Mgandilwa amefanya ziara katika Ofisi za TANESCO wilaya ya Kigamboni.

Mkuu wa wilaya ya Kigamboni Mh Hashim Mgandilwa akizungumza na wafanyakazi TANESCO

Baada ya kutembelea Ofisi mbalimbali na kujionea hali halisi ya utendaji kazi alizungumza na uongozi na wafanyakazi wa taasisi hiyo.

DC Mgandilwa pamoja na kuwapongeza wafanyakazi kwa juhudi zao za kila siku kuboresha huduma za upatikanaji wa umeme wilayani hapa, alikemea vikali mambo ambayo yanasababisha kuzorota kwa huduma hiyo mara kadhaa. 

Amewataka kuboresha mifumo ya umeme na kumaliza tatizo la kukatikakatika kwa umeme kila mara. Pia amesisitiza utoaji wa taarifa kwa wananchi kabla ya kukata umeme pale inapowalazimu kufanya hivyo kwa sababu za msingi.

Amewakumbusha wafanyakazi hao dhana ya uwajibikaji katika nafasi walizonazo ili kuwaletea wananchi maendeleo na kuwa yeye hatasita kumchukulia hatua za kinidhamu mtumishi yeyote atalayeleta uzembe na tabia zisizokubalika zenye kusababisha huduma mbovu kwa wananchi. 

DC Mgandilwa aliwataka viongozi wa taasisi hiyo kutengeneza ushirikiano mzuri na viongozi wa ngazi mbalimbali ili kurahisisha kuwafikia na kuwahudumia wananchi kwa wakati na kwa ufanisi mkubwa. 

Pia Mkuu wa wilaya amewataka TANESCO kuharakisha taratibu za ujenzi wa Ofisi za TANESCO wilaya ya Kigamboni zinazotarajiwa kujengwa eneo la Somangila na kusisitiza matumizi mazuri na sahihi ya pesa itakayotolewa kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi hizo. 
Mkuu wa wilaya ya Kigamboni (katikati) akipata maelezo kutoka kwa Meneja wa TANESCO mkoa wa Temeke Eng. Jahulula M. Jahulula aliyeko kulia, kushoto ni Meneja wa TANESCO wilaya ya Kigamboni Eng. Richard S. Widimael 



Katibu tawala wa wilaya ya Kigamboni Ndg Cosmas Hinju akizungumza katika kikao hicho





Sehemu ya wafanyakazi wakimsikiliza Mkuu wa wilaya